#Biashara

Ifahamu UTT-AMIS na Namna Inavyoweza Kukupa Faida

UTT AMIS

Unit Trust of Tanzania – Asset Management and Investor Services au kwa jina rahisi tunaita UTT-AMIS ni taasisi ya fedha iliyoanzishwa na serikali ya Tanzania kuwa suluhisho la uwekezaji kwa ajili ya watu binafsi na taasisi mbalimbali.

Kazi yake kuu ni kusimamia uwekezaji wa pamoja ambao huitwa mfuko wa pamoja wa uwekezaji. Mfuko wa pamoja wa uwekezaji unaruhusu watu kukusanya pesa zao kwa pamoja na kuwekeza katika vyombo tofauti tofauti vya uwekezaji kwa usimamizi wa wataalamu au washauri wa fedha na uwekezaji.

Kwa kufanya hivyo UTT-AMIS inaboresha na kuweka wepesi kwa watu wa kila namna kuweza kuwekeza na kutunza pesa kwa faida kupitia mifuko ya pamoja.

UTT-AMIS Inafanya Vipi Kazi?

Uwekezaji wa Pamoja

UTT-AMIS inafanya kazi kwa kukusanya pesa za wawekezaji wengi kwa pamoja na kuziweka kwenye mfuko mmoja. Kisha mfuko huu wa pamoja unasimamiwa na kutumika kitaalamu kuwekeza katika vyombo mbalimbali vya uwekezaji kama Hisa katika soko la DSE, Hatifungani za serikali, na(au) Treasury bills na fixed deposits mbalimbali.

Kwa kuwekeza kwa pamoja hata watu binafsi wenye kipato kidogo wanaweza kuwekeza katika sehemu zinazohitaji kipato kikubwa ili kuona faida. Kwahiyo wawekezaji wananunua vipande vya mfuko huu wa pamoja, na faida yao inalipwa kulinga na idadi na thamani ya vipande alivyo navyo.

Aina ya Uwekezaji ndani ya UTT-AMIS

UTT-AMIS ina rasilimali mbalimbali katika namna ya uwekezaji wake. Rasilimali hizo zinalenga kuwafikia/kubeba watu wenye malengo tofauti tofauti katika uwekezaji wao. Aina hizo za uwekezaji ni hizi

  • Wekeza Maisha Fund. Huu ni mfuko wa uwekezaji wa muda mrefu ambao unawalenga wawekezaji wenye lengo la kukuza vipato vyao kwa muda mrefu. Mfuko huu unawekeza katika equities na hatifungani za muda mrefu. Kwahivyo hii ina wafaa wawekezaji wenye uvumilivu mkubwa wa hatari na wanaweza kusubiri kupata faida kwa muda mrefu.
  • Jikimu Fund. Mfuko huu unawafaa wale wanaotaka kupata kipato cha mara kwa mara. Mfuko huu unajikita katika kutoa faida za mara kwa mara kupitia uwekezaji katika vyombo vinavyoongeza kipato kama vile hatifungani za serikali na hatifungani za kampuni binafsi. Mfuko huu unawafaa zaidi wastaafu na watu binafsi wanaohitaji matumizi ya mara kwa mara.
  • Ukwasi Fund / Liquid Fund. Ni uwekezaji wa muda mfupi na hatari ndogo unaotoa ukwasi mkubwa (high liquidity). Mfuko huu unajikita kuwekeza katika masoko ya fedha kama hatifungani za muda mfupi za serikali na fixed deposits. Hii inafanya mfuko huu kuwafaa zaidi wawekezaji ambao watahitaji pesa zao ndani ya muda mfupi kwa haraka na bila hatari kubwa.
  • Watoto Fund. Hii ni maalumu kwa ajili ya wazazi na walezi ambao wanataka kutunza fedha kwa ajili ya watoto wao huko mbeleni. Mfuko huu unalenga uwekezaji wa muda mrefu ukiwa na hatari kiasi.
  • Hatifungani Fund / Bond Fund. Mfuko huu unajikita katika uwekezaji wa vyombo ambavyo viko fixed kama hatifungani za serikali na kampuni binafsi. Mfuko huu unawafaa wawekezaji ambao wanapendelea hatari ndogo na faida zinazowafikia kila baada ya muda fulani kama vile mara mbili kwa mwaka.
  • Umoja Fund. Huu ni mfuko unaotoa usawa wa uwekezaji kati ya equities na fixed income securities. Huu upo kwa ajili ya wawekezaji ambao wanataka usawa katika kupata kipato mara kwa mara na kukuza kile walicho nacho. Hivyo hii inafaa kwa watu wenye malengo ya fedha yasiyo ya muda mfupi wala muda mrefu.

Kila mfuko wa UTT-AMIS una aina ya uwekezaji unaoweza kubeba malengo ya watu mbalimbali, hivyo kuwapa nafasi wawekezaji kuchagua mfuko unaoendana na malengo yao ya fedha.

Bei ya Vipande na Faida

Bei ya kila kipande katika kila mfuko inapangwa na Thamani Halisi ya Mali au Net Asset Value (NAV), ambapo bei hii inapatikana kwa kugawanya jumla ya thamani ya mali za mfuko (total value of the fund’s assets) kwa idadi ya vipande vinavyomilikiwa muda huo (number of outstanding units).

Ikiwa thamani ya mfuko inapanda na kushuka ndivyo ambayo NAV pia inapanda na kushuka, na hivyo kuathiri pia bei ya ila kipande cha katika mfuko husika. Wawekezaji wanaweza kupata faida kwa namna kuu mbili.

  • Capital Gains / Kupanda Thamani. Ikiwa bei ya kipande itapanda tangu muwekezaji aliponunua, kiasi kilichoongezeka ndiyo tunaita Capital Gain.
  • Distributions / Usambazaji. Haya ni malipo ya kila baada ya muda fulani yanayolipwa na baadhi ya mifuko kwa mfumo wa riba au dividend.

Faida za Kuwekeza Kupitia UTT-AMIS

  • Usimamizi wa Kitaalamu. UTT-AMIS imeajiri wasimamizi wa pesa wenye elimu na uzoefu wa kutosha ambao hufanya maamuzi ya uwekezaji baada ya kufanya utafiti wa kutosha na uchambuzi mzuri wa masoko. Hii inapunguza mzigo wa mtu binafsi kufanya tafiti yeye mwenyewe.
  • Diversification/Usambazaji kwa kuweka fedha kwenye mfuko wa pamoja. UTT-AMIS wanaweza kuwekeza katika mifuko mingi tofauti tofauti ili kupunguza hatari ya kupoteza pesa katika mfuko mmoja. Hata muwekezaji mdogo anapata faida kulingana na namna hii ya uwekezaji kitu ambacho ngumu kupata akiwa peke yake.
  • Affordability / Unafuu, UTT-AMIS inaweka wepesi kwenye uwekezaji ili hata mtu mwenye mtaji mdogo sana aweze kuwekeza.
  • Ukwasi / Liquidity, Kulingana na mfuko uliochagua, wawekezaji ndani ya UTT-AMIS wanaweza kupata pesa zao kwa haraka sana. Mfano mfuko wa Ukwasi umeundwa kwa namna ambayo unaweza kupata pesa zako haraka sana, hivyo inafaa kwa wanaofanya uwekezaji wa muda mfupi.
  • UTT-AMIS inadhibitiwa na CMSA. Capital Markets and Securities Authority (CSMA) wanahakikisha UTT-AMIS hawakiuki maadili na sheria za uwekezaji na wapo kulinda fedha za wawekezaji, hii ina maana kwamba wawekezaji wanalindwa sana na CMSA.

Hatari ya Kuwekeza na UTT-AMIS

  • Hatari kwenye masoko ya fedha. Kwa kuwa UTT-AMIS inawekeza katika equities na masoko mengine ya fedha, thamani ya vyombo katika masoko haya inaweza kubadilika muda wowote. Inaweza kupanda au kushuka. Kushuka kwa thamani ni hasara kwa wawekezaji.
  • Hatari ya Riba ya Benki Kuu. Uwekezaji katika hatifungani na fixed income una hatari ikiwa riba ya benki kuu itapanda. Riba hii inapopanda thamani ya hatifungani na fixed income inashuka na kushusha thamani ya mfuko wote pia.
  • Hatari kwenye Ukwasi. Wakati baadhi ya mifuko ya UTT-AMIS ina ukwasi mkubwa, mifuko mingine inaweza kuwa na udhibiti wa namna na muda gani pesa zinaweza kutolewa. Ni vyema muwekezaji ufahamu vizuri sheria zao za ukwasi kabla hujawekeza pesa zako.
  • Hatari ya Mfumuko wa Bei. Mfumuko wa bei unaweza kudanganya/kuondoa thamani ya kweli ya faida unazopata. Mfano ikiwa asilimia ya mfumuko wa bei inakuwa sawa au zaidi ya asilimia ya faida, basi muwekezaji unaweza kupata hasara katika uwezo wa kununua bidhaa.
  • Wasimamizi wa Mfuko. Ubora na faida ya UTT-AMIS unategemea sana maamuzi na uzoefu wa wasimamizi wa kila mfuko. Ikiwa wasimamizi watafanya maamuzi yasiyo sahihi basi ni rahisi sana kupata hasara.

UTT-AMIS ina umuhimu mkubwa sana katika kuboresha na kusogeza watu katika uwekezaji ndani na nje ya nchi ya Tanzania. Hii inawezekana kwa kuwa UTT-AMIS wanawekeza katika vyombo tofauti tofauti vya fedha na mifuko ina simamiwa na wataalamu waliobobea usimamizi wa fedha.

Wakati UTT-AMIS inatoa faida nyingi na uwekezaji nafuu ni vyema mtu ukafahamu hatari ya kuwekeza katika aina hii ya masoko ya fedha na pia ukafanya utafiti wako mwenyewe kabla hujawekeza katika kitu chochote.

Ifahamu UTT-AMIS na Namna Inavyoweza Kukupa Faida

AI Kuwa Mshauri wa Fedha kwa Vijana

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *