AI Kuwa Mshauri wa Fedha kwa Vijana Wenye Kipato Kidogo

Tangu ujio wa ChatGPT kumekuwa na kampuni nyingi zilizotoa Artificial Intelligence zenye malengo tofauti tofauti mengi, yote yakiwa kulenga kuboresha na kuimarisha maisha yetu ya kila siku.
Kuna AI za kutengeneza picha, video, kufanya tafiti mbalimbali, AI ambazo zimekuwa kama walimu, AI za ushauri wa kifedha na nyingine nyingi. Kila kampuni inataka kuwa kinara wa kutoa huduma fulani maalumu. Katika majukumu yote ambayo AI inaweza kubeba, nimevutiwa zaidi na kuitumia AI kama mshauri wa kifedha.
Lengo langu kama kijana wa kitanzania ni kutokuwa na madeni ya aina yoyote ifikapo mwishoni mwa mwaka 2025. Kwa kawaida mpaka sasa hivi kwa kipato kidogo nilicho nacho naishi kwa kuweza kula tu, ila ni ngumu kufanya maendeleo binafsi.
Niliwaza sana kuhusu kuwa na mshauri wa fedha binadamu, lakini huyu pia ataongeza gharama zangu za maisha. Sababu nitalazimika kumlipa na kumlipa pesa nyingi ambayo sina. Akili yangu ikaigeukia Artificial Intelligence ya openAI maarufu kwa jina la ChatGPT.
Ndani ya ChatGPT kuna aina nyingi za GPT ambazo baadhi zimeundwa maalumu kabisa kuwa mshauri wa kifedha, lakini lengo langu halikuwa kutumia hizo. Nilitaka kuona hii ChatGPT ya kawaida ambayo sio ya kulipia itaweza kunipa uelekeo unaoweza kunisaidia.
Kuipa ChatGPT Scenario ya Kijana wa Kitanzania
Kwanza nikaona ili tuelewane inatakiwa niiambie kabisa hali niliyo nayo kwa sasa. Kuanzia kipato ninachopata mpaka madeni. Basi prompt yangu ilikuwa hivi (data nilizotumia hapa si za kweli, ila zinaendana na maisha ya kijana wa Tanzania).
“Naitwa Charles ni kijana wa kitanzania ninayekaribia umri wa miaka 30. Leo nataka wewe uwe mshauri wangu wa fedha na nitakwambia kuhusu hali yote ya uchumi wangu. Kwa sasa mimi ni muajiriwa na mshahara wangu ni Tsh. 500,000. Nadhani naishi maisha ya gharama zaidi ya kipato changu. Nina biashara nyingine nafanya lakini hii haileti faida yoyote kwa sababu imeanza miezi miwili iliyopita. Kila siku natumia nauli kiasi cha Tsh. 3,000 na natumia Tsh. 3,500 kwa ajili ya maji ya kunywa na chakula mchana. Hapa nilipo nina mkopo usio na riba kiasi cha Tsh. 150,000. Bili ya umeme na maji kila mwezi inafika jumla ya Tsh. 50,000. Naishi peke yangu. Ninatamani kufikia mwishoni mwa mwaka 2025 nisiwe na madeni yoyote, na pia nataka kufungua biashara nyingine mwezi July 2025 ili niongeze kipato changu. Biashara hiyo itahitaji mtaji wa Tsh. 3,000,000. Unaweza kunisaidia vipi hapa.”
Baada ya muda wa kuzungumza na ChatGPT majibu yake yamenifurahisha na nimeona yanaweza kusaidia wengine wengi ikiwa mtu utaweza kufuatisha maelekezo na kusimamia vizuri pesa zako. Mazungumzo yote na ChatGPT hako hapa; ChatGPT kama mshauri wa uchumi binafsi.
Ilichonifurahisha ChatGPT ni uwezo wake wa kuchukua yale yote umeiambia na kuyatumia kukuelekeza mpango maalamu wa kukusadia kujikwamua kwenye shida ulizo nazo.
Kwanza ChatGPT imenipa matumizi yangu yote ya mwezi kwa ujumla kulingana na yale nimeiambia. Kisha ikanipa muhtasari na ushauri kuhusu hali yangu ya uchumi ya sasa kulingana na scenario niliyoiambia.
Baada ya ChatGPT kunipa majibu hayo nikaongeza kuiambia kwamba ninachangamoto nyingine ya kushindwa kulipa kodi ya mwezi uliopita mahali ninapoishi, na kwamba natamani kujua ni sehemu gani naweza kuwekeza ili niendelee kukuza kipato changu na kuondokana na maisha ya mbio za panya.
Moja kwa moja ChatGPT imenipa ushauri kuhusu kuwekeza katika Hisa za DSE na katika UTT-AMIS, lakini kulingana na hali yangu ya uchumi mahali pananifaa zaidi ni UTT-AMIS.
Na ikaenda mbali zaidi kuelekeza namna naweza kujiunga na faida ambazo nitazipata ndani ya UTT-AMIS.
Kitu naweza kusema ni kwamba mpaka sasa Artificial Intelligence imefika mbali sana katika kurahisisha maisha yetu ya kila siku. Ikiwa tutaweza kuzitumia kwa usahihi katika kuboresha maisha yetu ya kila siku basi tuna nafasi kubwa kama vijana kufanya mabadiliko ya maisha yetu.