Ni Kweli Teknolojia Imeshindwa Kumuondoa Dalali wa Nyumba?

Moja ya sekta yenye pesa na inayokua haraka sana Tanzania ni sekta ya majengo. Sekta ambayo watu muhimu ni madalali. Dalali ndiye mtu anayemuunganisha mteja na mmiliki wa jengo. Pamoja na kwamba dalali ana umuhimu wake kurahisisha hii biashara, ila bado wana changamoto moja kubwa mno.
Dalali huwa anadai kuchukua kodi ya mwezi mzima pale ambapo mteja anakubali kupangisha eneo husika. Si hivyo tu, bali huwa wataka kulipwa finders fee (pesa ya kutafuta eneo). Hizi gharama za kumlipa dalali ndizo zinakuwa kama kamisheni kwake kwa kufanikisha hii biashara.
Je, ni haki mteja kulipa hizi gharama?
Kiukweli asilimia kubwa ya watu wanachukizwa na hizi gharama, maana ni gharama kubwa mno kusema mteja azibebe peke yake. Hivyo watu wengi mtandaoni hulalamika na kila mmoja huja na mawazo yake ya nini kinaweza saidia.
Katika mawazo mengi moja limeonekana kuongelewa sana na baadhi ya watu wameshajaribu kulifanyia kazi. Wazo hilo ni kuunda app au website ambayo itakuwa na orodha ya nyumba zote katika eneo fulani na kiasi cha kodi katika nyumba hiyo.
Lengo likiwa kwamba mteja utaingia kwenye huu mfumo na kuchagua nyumba unayotaka na moja kwa moja utawasiliana na mwenye nyumba na kumalizana nae.
Kwa muda mfupi unaweza kuona hu ni utatuzi mzuri na utafanya kazi.
HAPANA huu si utatuzi kama ambavyo mmoja wa developers aliwahi kujaribu na akarudisha majibu haya. Anon Codex Link.
Changamoto ya huo utatuzi ni kwamba kuna uwezekano mkubwa biashara yako itafeli kulingana na ukosefu ya malipo ya kutosha kuendesha mfumo wako. Sababu hapa wengi watategema mwenye nyumba akilipwa kodi atakuja kukulipa wewe.
Itashindikana kwako sababu uwezekano mkubwa ni kwamba mwenye nyumba na mteja wakianza kuwasiliana ni rahisi sana kukuondoa wewe kwenye hiyo biashara na wao kumalizana moja kwa moja.
Suluhisho la Hii Changamoto
Tunachohitaji kuwa nacho ni mfumo wa biashara unaofanya kazi kwa pamoja na madalali na wamiliki wa haya majengo. Aidha ufanye kazi na dalali au umuondoe kwa ujumla yote yanawezekana. Pamoja na kwamba yote yanawezekana bado kuna gharama huwezi kuzikwepa.
Gharama kama ya dalali kuchukua kodi ya mwezi mzima ni kiwango ambacho kipo duniani kote si Tanzania peke yake. Unachoweza kufanya ni labda kupunguza tu kiasi.
Sasa cha kwanza unatakiwa kufanya ni kuwa na mkataba baina yako na wenye majengo. Mkataba ambao unamtaka mwenye jengo akabidhi kila kitu kwako (kwenye agency/kampuni yako). Kukabidhi kila kitu ni kwamba anakupa mpaka funguo za nyumba.
Hivyo wewe ndiwe mwenye mamlaka ya kufanya matangazo mpaka kwenda kumuonyesha mteja jengo husika. Ni vile unakuwa dalali ila tu si kama hawa wa kawaida. Ndani ya mfumo wako mtu anaweza kuona nyumba zinazopatikana kwa urahisi na kuona hata picha za nyumba hizo.
Makubaliano yako na mmiliki ni kwamba hata mmiliki akifuatwa na mteja moja kwa moja anamuelekeza mteja kwenye mfumo wako na huko ndiko atakamilisha kila kitu.
Commision yako utaipata kupitia malipo ambayo mteja atafanya kwako kabla hujaenda kumkabidhi kwa mwenye nyumba.
Lakini kama mkataba ukikaa vizuri zaidi basi mnaweza kubaliana kwamba hata usimamizi wa nyumba kusimamia malipo ya kodi na mengine yanakuwa juu yako. Ambapo wewe utalipwa kwa asilimia kadhaa ya kodi kila mwaka.
Mfano mwanzo kabisa unachukua asilimia 20% ya jumla ya kodi ya mwaka mzima au unachukua asilimia 80% ya kodi ya mwezi mmoja. Ikiwa utasimamia mambo mengine yote wewe mwenyewe basi utakuwa unachukua asilimia 15% ya jumla ya kodi ya mwaka mpaka pale mkataba unapofikia ukomo.
Ili kufanikisha biashara ya namna hii kwa hapa Tanzania unahitaji kuwa na vitu vikuu viwili.
- Ukiritimba/Monopoly. Uweze kuukaba mfumo wote uwe chini yako. Dalali wa mtaani asihusike kabisa.
- Pesa. Uwe na pesa ya kutosha kufanya matangazo na kuwa na ushawishi.
Ukiweza kuwa na mambo hayo mawili basi itakuwa rahisi sana kwako kufanikisha hii biashara.