Huwezani na Biashara ya Milioni 10 Kama Ilivyo ya 10,000

Ukisoma vitabu utaambiwa ukiweza kuendesha biashara inayokupatia kiasi cha Tsh. 10,000 kwa wiki, basi utaweza kuendesha biashara inayokupa milioni 100 kwa wiki. Je, kuna ukweli katika kauli hii?
Binafsi sioni kama kauli hiyo ni ya kweli katika uhalisia. Maana naweza kukukwambia fanya biashara fulani itaweza kukupa milioni 1 kila wiki, ila kama wewe si mtu sahihi kuendesha biashara hiyo na huna hujuzi wa kutosha basi hautaweza kupata kiasi hicho cha pesa.
Uhusiano wa biashara na mwenye biashara ni kama uhusiano wa gari na dereva. Mfano leo hii ikiwa tayari unajua kuendesha gari, ukipewa gari kama IST utaweza kuendesha bila shida. Na ukipewa zile gari za mashindano ya Formula one uwezekano mkubwa ni hautaweza kusogea hata mita 1.
Hapo ndiyo utofauti ulipo kati ya gari ya milioni 20 na gari ya bilioni 3.6. Ndivyo ilivyo hata kwenye biashara. Mara nyingi ukiingia mtandaoni utasiki fanya Forex inalipa, fanya dropshipping au kuwa freelancer na kazi nyingine nyingi za mtandaoni.
Ndani ya muda mfupi unaweza kujikuta umeshajaribu zaidi ya biashara 3 na zote hujapata mafanikio. Mwisho wa siku unakuja kuanza kulaumu kwamba kazi za mtandaoni hazina pesa. Wengine wanajaribu kuingiza bidhaa toka nje na kuuza Tanzania, na wengine wanaanzisha biashara fulani kwa sababu mwingine amefanya na kufanikiwa.
Sasa kama katika biashara hizo hizo wengine wamefanikiwa na wewe ukafeli. Je, shida ni wewe au biashara yenyewe?
Katika biashara ikiwa kuna walau watu 10 waliofanya na wakafanikiwa, basi hiyo biashara inawezekana ni sahihi. Wewe ukifeli basi huende shida ni wewe. Kama ambavyo ili kuendesha gari ya Formula one kuna ujuzi fulani lazima uwe nao tofauti na ule wa kuendesha IST, ndivyo ilivyo kwenye biashara.
Ukiwa na ujuzi wa kuendesha biashara ya kukupa Tsh. 10,000 kwa wiki, sio rahisi kwako kuendesha biashara ya kukupa milioni 1 kwa wiki. Kuna uwezekano mkubwa hiyo biashara itakufa mikononi mwako au kukufilisi.
Unachotakiwa kufanya ni kuendelea kujifunza kila siku na kukuza ujuzi wako polepole mpaka ifike wakati wa kuweza endesha biashara ya kipato kikubwa ndani ya muda mfupi. Hivyo ni sawa kusema mara nyingi shida si biashara, bali ni mwendeshaji wa hiyo biashara.