Kutoka Gengeni Mpaka Mauzo Mtandaoni: Namna ya Kuwa na E-Commerce Site Afrika

Katikati ya kelele za soko la Kariakoo na magenge yake wauzaji wa nguo, vifaa vya elektroniki, kompyuta na vitu vingine vingi wanataka kuuza mtandaoni. Wauzaji hawa na wengine wengi Afrika wanatamani kuongeza mauzo kwenye biashara zao. Wachache wameanza kuona kwamba kuwa na E-Commerce ni sahihi ili kukuza mauzo yao.
Mwaka 2025 mauzo ya bidhaa mtandaoni hapa Afrika yanakadiriwa kufikia $75 billion, inaonyesha kwamba nafasi za kukuza na kuanzisha biashara zimekuwa nyingi sana. Tatizo ni kwamba kuwa na biashara mtandaoni au kuwa na duka la mtandaoni kuna changamoto kadhaa. Andiko hili litakupa maelekezo sahihi kabisa ili kuifanya biashara yako kuwa hadithi yenye mafanikio ya mtandaoni.
Chagua Msingi wa E-Commerce yako
Wakati unafikiria kuanzisha biashara mtandaoni kitu cha kwanza ni kujua jukwaa lipi utalitumia kwa ajili ya biashara yako. Kama ambavyo huwa unatafuta eneo sahihi kwa ajili ya baishara yako. Hata mtandaoni iko hivyo pia.
Inafaa upate jukwaa ambalo linakidhi mahitaji yako, bajeti, na malengo yako ya kukuza biashara. Sio tu kuanzisha biashara katika platform yoyote ile bila msingi unaoleweka.
Majukwaa yaliyozaliwa Afrika yameonyesha kuwapa wafanyabiashara mafanikio makubwa na wateja kufanya waamini kununua mtandaoni. Mfano Jumia na Jiji wanatoa fursa nzuri kwa wafanyabiashara kuuza bidhaa ndani ya majukwaa yao.
Unapochagua kuuza kwenye majukwaa haya moja kwa moja unapata wateja ambao tayari wanaamini jukwaa hilo na wana uzoefu wa kununua bidhaa mtandaoni.
Kutumia majukwaa ambayo yameundwa maalumu kwa ajili ya Afrika kuna faida zake kadhaa. Faida yake kuu ni kwamba majukwaa haya tayari yanakuwa na njia za malipo za Afrika kama M-Pesa au Mixx by Yas.
Mifumo yao ya usambazaji bidhaa kufika kwa mteja inakuwa rafiki maana wanaelewa changamoto za usafirishaji ndani ya Afrika. Pia unakuwa na wateja wa Afrika ambao tayari wanatumia jukwaa hilo.
ZINGATIA: Wakati majukwaa ya Afrika yana faida zake kwenye kupata wateja na njia za malipo, bado haya majukwaa yana changamoto ya kuwa na kamisheni kubwa mno na hakuna uhuru wa kuweka muonekano unaotaka wewe.
Majukwaa ya Kimataifa Yanayofaa Afrika
Majukwaa kama Woocommerce na Shopify yanatoa mbadala mzuri sana katika kutengeneza E-Commerce. Haya yanatoa uhuru mkubwa wa kuweza fanya customization, lakini pia yanakupa nafasi ya kuongeza namna za kufanya malipo zile unazotaka wewe kwa makato nafuu zaidi.
Njia za Kufanya Malipo
Katika bara ambalo malipo kwa njia ya simu yametawala, namna ya malipo unayochagua kuwa nayo inaweza kuinyanyua au kuua biashara yako mtandaoni. Kitu cha msingi na rahisi ni kuweka njia ya malipo ambayo wateja wako tayari wanatumia na wanaiamini.
Njia ya Afrika ni malipo kwa njia ya simu. Afrika Mashariki tunatumia zaidi M-Pesa wakati Afrika Magharibi wanatumia MTN na Francophone Afrika wanatumia Orange Money.
Kwa Afrika hata baada ya kutatua changamoto ya malipo bado kuna changamoto ya usafirishaji wa Last Mile. Last mile ni usafirishaji wa mwisho wa kumfikia mteja wa mwisho.
Kutatua Changamoto ya Last Mile Delivery
Changamoto ya Afrika ni miundombinu ya usafirishaji kutokuwa na ubora na urahisi wa kufikika nyumba kwa nyumba na mtaa kwa mtaa. Unawezaje kusafirisha bidhaa katika miji ambayo mara nyingi mitaa yake haina majina? Au kufikisha vijijini ambako hata kukuta mitaa ni ngumu na anwani hazipo?
Kuna njia mbadala zimekuwepo Afrika. Mfano kwa mijini, huduma ya boda boda imekuwa uti wa mgongo wa usafirishaji kwa nchi kama Tanzania, Kenya na Uganda. Kwa vijijini wafanyabiashara wengi wamechagua kuwa na mawakala kwenye center za vijiji. Ambapo mizigo huwa inafika kwa hawa mawakala na mteja anaenda kupokea hapo mzigo wake. Na wakati mwingine mabasi ya vijijini yanatumika kama mawakala wa hawa wafanyabiashara.
Kufanya Matangazo kwa Muktadha wa Afrika
Kutangaza biashara yako Afrika kunahitaji uwe na mchanganyiko wa mtu mwenye ufahamu & kupenda teknolojia, lakini pia uwe na hekima ya kitamaduni za Afrika. Aplikesheni ya Whatsapp Business imekuja kama kifaa muhimu kwa wafanyabiashara kuweza simamia biashara zao.
Watu wa Afrika kwa asilimia kubwa wanaamini Whatsapp kuliko mitandao mingine. Hata kama mtu ataona tangazo kwenye mitandao ya kijamii au kuona bidhaa kwenye website, bado mtu atataka kuwasiliana na wewe Whatapp ndipo alipie bidhaa.
Kuanzisha E-Commerce yako mwenyewe unahitaji kuwa na domain ambayo unaweza nunua kwa Tsh. 30,000, gharama za hosting ambazo kwa mwaka huwa ni Tsh. 200,000, na SSL certificate.
Muhimu ni uanze polepole na kukuza biashara kadiri unavyozidi kwenda.
E-commerce kwa Afrika inakua haraka sana hasa ukizingatia malipo kwa njia ya simu yanazidi kutumika na watu wengi sana. Biashara yako mtandaoni inaweza kuanza padogo na ikakua polepole, lakini itaendelea kukua kulingana na msingi unayoiwekea biashara hiyo.