Logo Inatakiwa Kuwakilisha Inachofanya Biashara Yako?

Mara nyingi mtu anayeanzisha biashara na kutafuta kutambulika kwa wateja wake hubaki kujiuliza namna logo yake inatakiwa kuwa. Iwapo ifananen moja kwa moja na kile kitu anachofanya au iwe tu ya kipekee yenye kutambulika kwa urahisi?
Swali hili huwa na majibu tofauti tofauti kulingana na nani haswa unamuuliza na katika muktadha upi. Jibu jepesi la swali hili naweza kusema ni HAPANA logo si lazima ifanane moja kwa moja na kile unachokifanya au kile biashara yako inafanya. Jibu refu nitalitoa kulingana na mazingira ya biashara na nani unamuuliza.
Kulingana na nani unamuuliza
Graphics Designer
Graphics designer wako atakwambia logo yako inatakiwa iwe na sifa kuu tatu, iwe rahisi kukumbukwa, iwe ya kipekee na ifae kuwakilishwa kwenye jamii. Hii ni kwa sababu graphics designer anataka kutoa logo ambayo kwa mbali sana inahusiana na kile biashara yako inafanya, kuliko kuonyesha moja kwa moja nini biashara yako inafanya. Kwa kufanya hivyo ni rahisi logo yako kukumbukwa na watu na inaleta upekee ikiwa biashara unayofanya pia kuna wengine wanafanya na wao pia wakawa na logo kama yako.
Mfano umepita kwenye hardware ngapi Tanzania ukaona logo zinazolingana? Unakuta wengi logo zao zina chepe, gia na kofia ngumu ya mafundi. Kisha rudi angalia kampuni kubwa za simu kama Samsung, Apple na Huawei. Je, wote wangeweka kitu kinachoendana na wanachofanya tungeweza kutofautisha?
Mmiliki wa Biashara
Mara nyingi wamiliki huwa wanataka logo inayoonyesha wazi ni kitu gani wanafanya. Chukulia wamiliki wa biashara ndogo kama dada zetu wenye saluni za urembo. Wao huwa wanataka logo ionyeshe msusi akifanya kazi au kuonyesha mkono wa mdada akipakwa rangi kwenye kucha.
Ni baada ya muda tu kupita na wao kuwa wamepata jina ndipo wanaanza kutamani kubadili logo. Hapo wanaanza kutamani kuwa na logo ya kipekee inayotambulika na kuaminika na wateja wake ili aweze kujitofautisha na wengine.
Wateja
Logo tunaunda kwa ajili ya mteja na sio kwa ajili ya mfanya biashara au graphics designer. Hawa wawili wanafahamu wao kwanini logo iko vile ilivyo na inamaanisha nini kwao.
Kwa mteja anachohitaji ni kuona kitu anachokitambua kinahusiana na kampuni anayotaka na awe anaiamini. Yeye wala hawazi kitu kinachowakilisha moja kwa moja nini kampuni inafanya au haifanyi. Ingawa wakati mwingine mteja anachanganyikiwa na anakosa imani ikiwa logo inawakilisha moja kwa moja kile ambacho kampuni inafanya.
Kwa mteja logo inatakiwa akiona itoe hisia fulani kwake ya kutambua na kufurahia kwa kuwa tayari hii kampuni ameona inatoa huduma au bidhaa sahihi kwake. Mfano Nike wana ile alama ya TIKI. Je inaonyesha wanauza viatu? Hapana, ila mtu akiiona tu anatambua ina maana gani.
Kulingana na Mazingira
Biashara Ndogo/Inayoanza
Kwa biashara inayoanza au Biashara ndogo mara nyingi ni vyema logo ya mwanzo ionyesha kwa kiasi fulani kampuni inajihusisha na huduma au bidhaa gani. Hii ni kwa sababu bajeti ya matangazo kwa biashara ndogo huwa hafifu. Hivyo logo yako itakusaidia kutangaza kile unachofanya.
Mfano biashara ya upishi unaweza weka picha ya mpishi akiwa ameshika mwiko na vijiko. Hii haina maana kwamba logo hii utaitumia milele. Mbeleni kampuni ikishakuwa na jina kubwa na inatambulika unaweza kubadili logo. Moja sababu inaweza kuwa utambulike kwa urahisi au ikiwa utaanza kujihusisha na vitu vingine ambavyo havihusiani moja kwa moja na biashara ya mwanzo ila viko ndani ya kampuni moja.
Kampuni kubwa
Kampuni kubwa zinaweza kutumia logo zisizo na mambo na hazihusiani na kile wanachokifanya. Hii ni kwa sababu wao tayari wana wateja na wanatambulika kwa urahisi. Kampuni zinaangalia kujitangaza kwa kutumia uzoefu wa wateja wao kwao, na nini wateja wanaona kwao na sio moja kwa moja logo kuonyesha kile ambacho kampuni yao inafanya.
Mfano kampuni kubwa zinazotumia maneno tu kama Google au Jeep. Au alama ya Tufaha (Apple) iliyong’atwa kwenye logo ya kampuni ya simu na computer ya Apple.
Logo si lazima ihusiane moja kwa moja na kile ambacho kampuni yako inafanya, lakini kwa asilimia kubwa inategemea na muktadha wa uhitaji wa hiyo logo. Biashara ndogo zinaweza kufaidika na logo ambayo inahusiana moja kwa moja na kile wanachofanya, wakati kampuni kubwa zinafaidika zaidi na logo ambazo ni rahisi kukaa akilini na hazifanani na yoyote yule.
Muhimu ni utambuzi wa logo uendane na utambuzi wa kampuni, iwe logo inahusiana moja kwa moja na kile ambacho kampuni au haihusiani.