Ni Kweli Marekani Walifika Mwezini?

Marekani hakuwahi kwenda mwezini. Apollo 11 haikuwa kweli. Binadamu hajawahi kufika mwezini. Bila shaka umewahi kusikia moja wapo kati ya hayo, sio?
Kumekuwa na nadharia nyingi sana kuhusu binadamu kufika mwezini kwa miaka 50 iliyopita tangu Neil Armstrong na Buzz Aldrin walipokanyaga mwezi kwa mara ya kwanza. Hii ilikuwa moja ya mafanikio makubwa sana ya NASA, ambayo mpaka leo yanaleta wasiwasi.
Dunia ya sasa ni kama vile tunaishi kwenye bahari ya taarifa. Kwa miaka 5 iliyopita kumekuwa na ongezeko kubwa sana la taarifa kuzidi miaka 1000 iliyopita ya mwanadamu. Vitu pekee tulivyo navyo na tunaweza kutumia kujua ukweli na usahihi wa taarifa ni uwezo wetu wa kufikiri.
Sasa je, ni kweli binadamu hakufika mwezini? Tuangalie baadhi ya vitu ambavyo vitakusaidia kufanya maamuzi.
Nadharia 1: Vivuli Kwenye Picha za Mwezini Vinaonyesha Picha ni za Uongo
Angalia hii picha hapa chini. Angalia namna vivuli vya Neil Armstrong na hiyo kama fimbo vimeonekana na useme ina shida gani?

Vivuli hivyo vinaonekana kama haviko sambamba.
Hii picha inatumika kama uthibitisho wa watu wenye nadharia kwamba binadamu hakufika mwezini. Ingekuwa kwamba jua ndilo lingekuwa kitu pekee kinachotoa mwanga mwezini basi ni sahihi vivuli ilifaa viwe sambamba.
Ila pia inawezekana wakiwa studio kutengeneza hii picha kulikuwa na vyanzo vingi vya mwanga. Ni sahihi inawezekana, ila haiko hivyo.
Kitu kama hiki kingeweza kutengenezwa hapa duniani bila shida yoyote. ila kuna wakati inatokea kwamba mistari iliyosambamba haionekani kuwa sambamba sababu ya mtazamo uliopo mtazamaji. Uzuri kitu kama hiki unaweza kukijaribu wewe mwenyewe.
Nenda nje jioni jua linapozama kisha jaribu kitu kama hicho utaona.
Nadharia 2: Astronauts wa Apollo Wasingepona Kwenye Mionzi Hatari ya Dunia
Dunia imezungua na anga lenye chembechembe zenye chaji. Anga hili linaitwa Mkanda wa Mionzi ya Van Allen.
Hili ni anga ambalo linabeba nguvu nyingi ya umeme ambao unakadiriwa kuwa 30keV au 30,000 Volts. Kwa nguvu ya kiasi hiki haikutakiwa kuwezekana kwa astronauts kuweza vuka hili anga na kwenda mwezini. Kujibu hili swali naomba nivute akili yako kuna picha uone.
Sufuria ikiwa ya moto na ukaishika bila kitambaa. Je, utaikumbatia? au unaishika haraka na kuiachia? Sufuria hiyo ukikumbatia lazima utaungua vibaya mno, lakini ikiwa unaishika tu ndani ya sekunde moja na kuihamisha sio rahisi kusikia maumivu ya ule moto.
Ndivyo ilivyo kwa safari ya kwenda mwezini. Kwa kuwa unatakiwa kupita kwenye anga hili kwa spidi kubwa ili usipate madhara ndivyo ambavyo Apollo 11 ilifanya. Na ni wazi ilifaa wawe na spidi kubwa maana unapooenda ni mwezini na ili ufike lazima uweze kuikataa nguvu ya mvutano ya dunia.
Nadharia 3: Kwanini Hakuna Nyota Kwenye Picha za NASA za Mwezini?
Watu wengi huwaza kwamba kwakuwa walipiga picha mwezini basi ilifaa nyota zionekane kwa wingi. Hasa ukizingatia kwamba mwezini hakuna mawingu ya kusema yanazuia picha isionekane.
Kwenye hizi picha wale astronauts na ardhi ya mwezi vinaonekana kumulikwa sana na jua. Kwahivyo ni kama kusema kwa muda picha zinapigwa mwezini ilikuwa mchana.
Kukiwa na mwanga mwingi hivyo wa mchana, umewahi kupiga kupiga picha na nyota zikaonekana?
Nadharia 4: Kama Kweli Walienda Mwezini Kwanini Hawajaenda Tena?
Apollo mission ya mwisho kufika mwezini ilikuwa mwaka 1972. Labda hii ni kwa sababu hatujawahi kabisa kwenda mwezini?
Apollo 17 haikuwa kikomo cha kutaka kwenda mbali na anga la dunia. Miaka yote iliyoendelea binadamu tumeendelea kujaribu kuweka kambi nje ya anga la dunia.
Lakini pia Marekani alikuwa ameshinda vita ya kisiasa ya kupeleka watu mwezini na hilo ndilo lilikuwa lengo kuu la mwanzo. Kwamba Marekani awe wa kwanza kufikisha watu kwenye mwezi. Hivyo baada ya mwezi nguvu yote ikaelekezwa kwenye International Space Station ambayo imekuwa ikihifandhi watu tangu mwaka 2000.
Hivyo ni sawa kumaliza kwa kusema Apollo 11 mission ilikuwa kweli. Binadamu amewahi kufika mwezini na tuna picha na video nyingi za kuthibitisha hayo.