Zifahamu Bonds/Hatifungani na Namna Zinavyoleta Faida

Bonds/Hatifugnani ni aina ya soko la fedha ambalo serikali na baadhi ya kampuni hutumia kukopa fedha za uwekezaji kutoka kwa wananchi na wawekezaji mbalimbali. Hatifungani kwa lugha rahisi ni mkataba ambao anayetoa hatifungani anaahidi kurudisha pesa yako yote (Principal Amount) pamoja na riba (interest coupons) ambayo inalipwa kila baada ya miezi kadhaa kwa kipindi cha muda fulani (Maturity date).
Hatifungati ni kifaa muhimu sana kwenye uchumi wa nchi na kampuni, kwa sababu zinasaidia taasisi hizi kuweza kukamilisha miradi mikubwa au kufikia malengo ya bajeti waliyopanga kwa wakati. Kwa Tanzania hatifungani zinatumika sana na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupita Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na mara chache zinatumika na taasisi binafsi hasa za kifedha kama CRDB.
Hatifungani Zinafanya Vipi Kazi
Hatifungani zinapotangazwa na muwekezaji akanunua hatifungani kadhaa, moja kwa moja muwekezaji huyu anaikopesha taasisi iliyotangaza hizo hatifungani. Baada ya kununua hatifungani, muwekezaji anategemea mambo haya kutoka kwa taasisi iliyouza hatifungani hizo.
- Taasisi italipa riba ya hatifungani hiyo kila baada ya muda fulani kulingana na makubaliano mpaka pale hatifungani hiyo inapofikia mwisho wa mkataba wake (Maturity period).
- Taasisi italipa pesa yote iliyowekezwa mwanzo mara tu hatifungani inapofikia ukomo wake.
Mfano serikali ya Tanzania ikatangaza hatifungani za miaka 10 zikiwa na coupon rate (riba) ya 10%. Muwekezaji atakayenunua hatifungani za Tsh. 1,000,000 atapokea riba ya 10% kila mwaka ambayo ni sawa na Tsh. 100,000 kwa mwaka mpaka miaka 10 itakapoisha. Na mwisho wa miaka 10 serikali italipa ile Tsh. 1,000,000 aliyoweka muwekezaji ule mwaka wa kwanza. Ni sawa kusema Muwekezaji atakuwa kapata faida ya Tsh. 1,000,000 ndani ya miaka 10 na ile Tsh. 1,000,000 yake bado inakuwepo.
Mambo Muhimu Kwenye Hatifungani
- Pricipal (Face Value), Hiki ni kiasi cha mwanzo kabisa unachowekeza kwenye bonds. Kiasi hiki kinakuja kulipwa mwishoni kabisa hatifungani inapofikia ukomo (maturity period)
- Coupon Rate, Hii ni riba ya mwaka unayolipwa kwa asilimia ya Face Value uliyoweka mwanzo.
- Maturity Date, Hii ni tarehe ambayo unalipwa ile principal amount ya mwanzo kabisa. Hii ndo siku ambayo bond inafikia ukomo wake.
- Yield, Riba halisi inayotokana na hatifungani, ambayo inaweza kubadilika kulingana na bei ya sasa ya hatifungani sokoni.
- Issuer / Taasisi, taasisi ambayo inatoa bonds ili wawekezaji waweze kununua, mfano Serikali ya Tanzania.
Aina ya Hatifungani Zilizopo Tanzania
Hatifungani za Serikali
Hatifungani za serikali mara nyingine huitwa hatifungani za hazina, hizi hutolewa na serikali ili ikusanye pesa kwa ajili ya kuwekeza miradi ya kijamii kama miundombinu, elimu na afya.
Kawaida hatifungani za serikali hufikia ukomo kati ya miaka 2 hadi miaka 25 na malipo yake ya riba (coupon payment) huwa mara 2 hadi 4 kwa mwaka. Hatifungani za serikali tunasema ni za hatari ndogo (low risk) kwa sababu zinatolewa na serikali.
Mfano serikali ya Tanzania inaweza kutangaza bond za miaka 5 zenye coupon rate ya 12%. Wawekezaji wanaonunua bond hizi watalipwa mara 3 kwa mwaka kila baada ya miezi 4. Principal amount italipwa baada ya miaka 5.
Hatifungani za Kampuni Binafsi
Hizi mara nyingi hutolewa na kampuni ambazo zinataka kukuza biashara zake, kuboresha ufanyaji wake wa kazi au kulipa madeni waliyonayo. Hizi ni tofauti na hatifungani za serikali kwa sababu hatifungani za taasisi binafsi zina hatari kubwa zaidi kuliko zile za serikali. Hizi zinategemea sana uchumi wa hizi kampuni kuendelea kuwa sawa.
Hatifungani za kampuni binafsi zina riba kubwa zaidi ya zile za serikali ikionyesha kwamba zina hatari kubwa pia. Ukomo wake huwa kati ya mwaka 1 mpaka miaka 10. Pia wakati mwingine huwa zina chaguo la kubadilishwa kuwa hisa.
Hatifungani za Manispaa
Hizi hutolewa na serikali za mitaa kama manispaa iki kuboresha miundombinu ya mitaa au vijiji. Kwa Tanzania bonds za namna hii ni nadra sana kuwepo ila zina umuhimu katika kusaidia ukuaji wa serikali za mitaa.
Hizi mara nyingi riba zake hazina kodi ili kushawishi wawekezaji wengi kuwekeza kwenye hizi na zina lengo kuu kuboresha serikali za mitaa.
Hatifungani Bila Riba / Zero Coupon Bonds
Hizi huwa hazina riba ya hata asilimia 1. Kinachofanyika ni kwamba hizi huuzwa kwa bei ya chini tofauti na thamani yake, lakini zinapofika ukomo unalipwa kulingana na bei yake halisia iliyotakiwa kuwepo. Utofauti kati ya bei ya manunuzi na kiasi unacholipwa ndiyo faida ya aina hii ya hatifungani.
Mfano serikali ikatangaza aina hii ya bond ya miaka 3 kwa thamani ya Tsh. 1,000,000 lakini wakauza kwa bei ya Tsh. 600,000. Inapofikia ukomo wa miaka 3 wewe utalipwa Tsh. 1,000,000 na utachukua hiyo Tsh. 400,000 kama faida ya uwekezaji wako.
Kwanini Uwekeze Kwenye Bonds?
Kwa muwekezaji ambaye anataka kutanua wigo wake wa uwekezaji basi bonds ni sehemu moja wapo ya kuwekeza kulingana na faida zilizopo ndani yake.
- Zinaongeza kipato chako. Kwakuwa bonds hulipwa kila baada ya muda fulani basi inakuwa rahisi kwako kupata fedha za kujikimu kila baada ya muda fulani.
- Zinakusaidia kutunza pesa zako wakati zikiendelea kukulipa riba.
- Ni uwekezaji usio na hatari kubwa hivyo ni nzuri katika kukuza maeneo ya uwekezaji.
- Unaweza kuzitumia kama dhamana ya kuchukulia mikopo benki.
Hatari Iliyopo Kwenye Kuwekeza Kwenye Bonds
- Ikitokea riba ya benki kuu imepanda, thamani ya hatifungani amabazo tayari zipo sokoni inashuka, kwa sababu hatifungani mpya zitakuwa na riba kubwa zaidi.
- Hatifungani za kampuni binafsi zinahatari kubwa hasa ikitokea kampuni inafilisika na kushindwa kulipa madeni yake.
- Mfumuko wa bei unaweza kusababisha malipo ya mara kwa mara ya riba yasiwe na faida ikitokea bei za bidhaa nchini zimepanda kuliko kawaida.
Kwa Tanzania hatifungani zina umuhimu sana katika uchumi wa nchi kwa sababu ni njia ya kuaminika kwa serikali kupata pesa za kuendeleza miradi yake. Kwa wawekezaji hatifungani huwa ni njia salama zaidi ya kuwekeza pesa zao na kutunza utajiri wao.
Hatifungani ni salama zaidi kuliko hisa, kwa sababu zina hatari ndogo na malipo yake huwa ni ya uhakika. Kuelewa aina tofauti tofauti ya bonds na namna zinafanya kazi inawasaidia watanzania kujua sehemu sahihi ya kuwekeza ikiwa wanataka kukuza kipato chao, kutunza pesa au kuongeza uwekezaji wao.
Hatifungani unaweza kununua kupitia soko la hisa la DSE au kupitia UTT-AMIS.